Top Ad unit 728 × 90

Uraia katika Jamhuri ya muungano wa Tanzania kutoka katika Rasimu ya katiba inayopendekezwa [Habari]

Uraia wa Jamhuri yaMuungano

65.-(1) Mtu ambaye, kabla ya Katiba hii kuanza kutumika, ni raia wa Jamhuri ya Muungano ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano.
(2) Uraia wa Jamhuri ya Muungano ni wa aina mbili na utapatikana kwa njia ya kuzaliwa au kuandikishwa.
Haki ya uraia 66. Kila raia ana haki ya kutambuliwa uraia wake na kwa madhumuni haya, mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha raia kupata hati ya kuzaliwa, kitambulisho cha uraia wake bila ya upendeleo na ubaguzi wa aina yoyote, na pale inapohitajika, nyaraka za kumwezesha kusafiri.
Uraia wa kuzaliwa
67.-(1) Kila mtu aliyezaliwa Tanzania Bara au Zanzibar atakuwa raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano iwapo, wakati wa kuzaliwa, mama au baba yake ni, au alikuwa raia wa Jamhuri ya Muungano.
(2) Kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, mtu aliyezaliwa nje ya Tanzania atakuwa ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa kuzaliwa kuanzia tarehe ya kuzaliwa kwake ikiwa mama au baba yake ni raia wa Jamhuri ya Muungano.


(3) Endapo mmoja kati ya wazazi wake alifariki kabla ya mtu huyo kuzaliwa, uraia wa mzazi huyo wakati wa kifo chake unatumika, kwa madhumuni ya kutambua uraia wa mtu huyo aliyezaliwa baada ya mzazi aliyefariki kana kwamba mzazi huyo alikuwa anaishi hadi kuzaliwa kwa mtu huyo.
(4) Mtoto mwenye umri chini ya miaka saba akikutwa ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano katika mazingira ambayo wazazi wake hawajulikani, atachukuliwa kuwa ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa kuzaliwa.
(5) Endapo uraia wa wazazi wa mtoto aliyepewa uraia chini ya masharti ya ibara ndogo ya 


(4) utabainika kuwa si uraia wa Jamhuri ya Muungano, uraia wa mtoto huyo utasita.
(6) Bila kuathiri masharti ya Ibara hii, Bunge litatunga sheria ambayo
itaweka masharti na utaratibu wa:
(a) upatikanaji wa uraia kwa watu waliozaliwa na raia wa Tanzania nje ya nchi;
(b) kurudisha uraia wa watu ambao uraia wao ulifutwa baada ya kupata uraia wa nchi           nyingine; na
(c) mambo mengine ambayo yatatakiwa kutungiwa sheria.

Uraia wa
kuandikishwa
68.-(1) Mara baada ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, mtu
ambaye amekuwa mkaazi wa Jamhuri ya Muungano na ambaye ametimiza masharti yote ya sheria za nchi anaweza kuomba kuandikishwa kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano.(2) Mtu aliyefunga ndoa na raia wa Jamhuri ya Muungano na ambaye:
(a) amedumu katika ndoa hiyo kwa kipindi cha miaka saba mfululizo; na
(b) ametimiza masharti yaliyoainishwa katika sheria kwa mujibu wa ibara ndogo ya (1),
anaweza kuomba uraia wa kuandikishwa kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano.
(3) Endapo ndoa iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) itavunjika,kama mtu huyo hakuukana uraia wake wa Tanzania, ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano.
(4) Mtoto aliyezaliwa katika ndoa iliyorejewa katika ibara ndogo ya (2), atakuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa kuzaliwa.
(5) Mtoto aliye na umri wa chini ya miaka kumi na nane ambaye wazazi wake si raia wa Tanzania, akiasiliwa na raia wa Jamhuri ya Muungano, kuasiliwa kwake, kutawezesha mtoto huyo kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa kuandikishwa.
(6) Bunge litatunga sheria, pamoja na mambo mengine, kusimamia masuala yanayohusu uraia wa Jamhuri ya Muungano.

Hadhi maalum ya 
watu wenye asili au nasaba ya Tanzania
69. Bila kuathiri masharti yaliyomo kwenye Sura hii, mtu yeyote
mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano kwa kupata uraia wa nchi nyingine, atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano, atakuwa na hadhi maalum kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.
Uraia katika Jamhuri ya muungano wa Tanzania kutoka katika Rasimu ya katiba inayopendekezwa [Habari] Reviewed by Unknown on Monday, October 27, 2014 Rating: 5

No comments:

All Rights Reserved by Dj Mchomo © 2014 - 2015
Powered By WordPress24x7

Contact Form

Name

Email *

Message *

Dj Mchomo. Powered by Blogger.